TANGAZO

ILI KUPATA TAARIFA ZA UHAKIKA KUHUSU MATANGAZO YA KAZI ZA MAENDELEO YA JAMII TEMBELEA BLOG HII KILA MARA Propellerads

Friday 11 November 2016

Hatua 7 za Kujifunza Kuandika CV


Kila mtu anaamini anaweza kuandika CV. Hata hivyo, changamoto kubwa ni kuweza kuandika CV itakayokuwezesha kuitwa kwenye usaili wa kazi.

Kumshawishi mwajiri akuite kwenye usaili katika soko la ajira lenye ushindani mkali si jambo la kulichukulia kwa wepesi kama wengi tunavyofanya.

Kuandika CV yenye tija mchakato unaohitaji maarifa sahihi, mpango na mwongozo wa kuandika CV kwa usahihi.

Mwandishi mashuhuri na mtaalamu wa menejimenti, W. Edwards Deming anatufundisha vema sana katika hili anaposema: “Kama huwezi kuelezea chochote unachofanya kama mchakato, basi hujui unachokifanya.”

Kumbe basi, ili ujue unachokifanya unapoandika CV ni lazima kwanza ujifunze jinsi ya kuandika CV.



Njia ya kwanza kujua hili ni kutambua Mbinu 3 za Kuandika CV Itakayozaa Usaili wa Kazi.

Ukishakuwa na mbinu za kuandika CV, sasa unatakiwa kujua hatua 7 za kuandika CV. Kwanini?

Kama unataka kujifunza kuandika CV kwa weledi, yafaa uanze kuacha kuandika CV kwa mazoea na kuchukulia zoezi la kusaka maarifa ya kuandika CV kama mchakato.

Kwanini ni muhimu kuzitambua hatua za kujifunza kuandika CV?

Leo hii kuna kila aina ya posti mtandaoni zinazojaribu kukuelekeza jinsi ya kuandika CV. Tatizo ni kwamba kila posti inazungumzia kipengele fulani au jambo fulani kuhusu uandishi wa CV. Hali hii, usipokuwa makini, inaweza kukuchanganya kwa sababu huwezi kujua umetoka wapi, unaelekea wapi katika kujifunza kwako.

Kama ambavyo miluzi mingi inavyomchanganya mbwa, ndivyo ambavyo miongozo mingi mtandaoni ya kujifunza kuandika CV inavyokuchanganya.

Na kama haitoshi, utapoteza muda wako mwingi sana kutafuta maarifa ya kuungaunga. Ni vigumu kubobea katika uandishi wa CV bila kuwa na utaratibu wa kujifunza hatua kwa hatua.

Kufuatia tatizo hili, posti hii inakuletea mwongozo kamili ambao utakuongoza kujifunza kuandika CV kwa utaratibu maalumu. Kwa maneno mengine, mwongozo huu ni mtaala wako unapojifunza kuandika CV.

Ni imani yangu kuwa mwongozo huu utakuwezesha kujifunza bila kutangatanga na hivyo kukuondolea usumbufu wa kurudiarudia mambo yaleyale, na pia utaokoa muda wako kwa kujifunza masomo sahihi tu.

Hatua ya kwanza unapoandika CV

Kwanini unataka kuandika CV? Ni swali la msingi kuanza nalo. Ni muhimu kutambua lengo la kuandika CV yako kabla kwa sababu hiki ndiyo kipimo cha ubora wa CV yako: CV utakayoandika ikishindwa kutimiza lengo lako la kuiandika, haiwezi kuwa bora hata kama imeandikwa kwenye karatasi la dhahabu.

Hatua ya pili unapoandika CV

Aina ipi ya CV itakufaa na kwanini? Jifunze kuchagua Muundo Sahihi wa CV ili muundo huo ukutumikie. Wengi wamekuwa watumwa wa muundo wa CV. Unachotakiwa ni kujifunza jinsi ya kuugeuza muundo wa CV kuwa mtumwa wako. Ndiyo! Muundo wa CV unatakiwa ukutumikie kutimiza malengo yako. Na utakapojua miundo mbalimbali na namna ya kutumia kila mmoja, utaweza kubadilika kulingana na mazingira kila mara utakapokuwa ukiandika CV yako.

Hatua ya tatu unapoandika CV


Namna ya kukabiliana na changamoto katika uandishi wa CV. Kutambua kuna changamoto zipi katika uandishi wa CV, na kisha, kujifunza namna ya kukabiliana nazo ni hatua muhimu sana katika kujifunza kuwa bingwa wa kuandika CV zitakazokuwezesha kuitwa kwenye usaili. Ni kama vile hospitali, daktari anaanza kutambua ugonjwa kisha anakabiliana nao. Fanya hivyo pia unapojifunza kuandika CV. Kwanza, tambua changamoto zilizopo, kisha jifunze jinsi ya kukabiliana nazo.

Hatua ya nne unapoandika CV


Katika harakati zako za kujifunza jinsi ya kuandika CV isiyoshindwa, ni muhimu ukajifunza kutambua “Mambo ya Kuzingatia Unapoandika CV.” Utakapojifunza orodha hiyo, utakuwa na dira ambayo itakuongoza kuandika CV yako kwa usahihi. Kumbuka kosa lolote kwenye CV yako litakutambulisha kwa mwajiri mtarajiwa kama mtu usiye makini.

Hatua ya tano unapoandika CV


Walimu karibu wote wa kuandika CV hufundisha vipengele au sehemu za CV. Lakini, kitu cha msingi ambacho wameshindwa kufundisha ni jinsi y kutumia kila kipengele cha CV kwa faida yako. Ni vema, ukajifunza maarifa haya ili uweze kuigeuza CV yako kuwa “tangazo la biashara” na kuibuka kidedea katika ushindani wa ajira.

Hatua ya sita unapoandika CV


Jambo lingine la msingi ambalo unapaswa kujifunza ni jinsi ya kuhakiki CV yako kabla ya kuituma kwa mwajiri. Kila mwandishi huwa na mpango wa kuhakiki kazi yake ya maandishi hata kama ameandika kujifurahisha. Hivyo, nategemea kwa mtu unayeandika CV uwe na plani nzuri ya kuhakiki CV yako kabla ya kuituma kwa mwajiri. Kwanini hatua hii ni muhimu? Kwa sababu CV ni nyenzo unayoituma kushindana na makumi kwa mamia ya CV nyingine ili uweze kuitwa kwenye usaili. Hivyo basi, unatakiwa kujifunza kufanya uhakiki wa CV yako kwa kutumiwa nyenzo ambazo zina uhakika wa asilimia 100%.

Hatua ya saba unapoandika CV


Hongera kwa kutambua hatua muhimu katika kujifunza kuandika CV za kiprofeshno. Lakini ngoja kwanza! Hivi umeishawahi kuona bondia anaingia ulingoni bila kujipima? Au, umewahi kujiuliza kwanini timu za mpira hutumia gharama kubwa kucheza mechi za kirafiki ili kujipima kabla ya pambano lenye ushindani mkali? NDIYO! Kujipima ni utimilifu wa kujifunza maarifa yoyote yale. Jifunze jinsi ya kujipima UBINGWA wako katika uandishi wa CV. Hakikisha unatumia kipimo na nyenzo ambazo zinaendana na unyeti wa elimu uliyojifunza. Hii itakuwezesha kuandika CV ambazo zitawachakaza washindani wako wote katika kila kazi utakayoomba.

No comments:

Post a Comment